12 Julai 2021 - 12:02
Wizara ya Ulinzi Afghanistan yaitaka Pakistan iache kuliunga mkono kundi la Taliban

Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imesema, kama serikali ya Pakistan inatiwa wasiwasi na hali ya usalama ya Afghanistan isitishe uungaji mkono wake kwa kundi la Taliban.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Afghanistan Fuad Aman ametoa kauli hiyo kujibu matamshi ya balozi wa Pakistan nchini humo aliyeviita "wanamgambo" vikosi vya kujitolea vya wananchi vinavyopambana na kundi la Taliban.

Aman ameongeza kuwa, watu waliojitolea kuvisaidia vikosi vya usalama vya Afghanistan si wanamgambo bali ni raia wa kawaida ambao wanapambana kurejesha amani na utulivu na kuilinda nchi yao.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Afghanistan amebainisha kuwa, hao ni watu wa Afghanistan ambao hawataki utawala wa Taliban urudi tena Afghanistan na nchi hiyo kurejeshwa kwenye historia ya giza iliyopita.

Fuad Aman amesisitiza kuwa ikiwa Pakistan inatiwa wasiwasi na hali ya usalama ya Afghanistan basi iache kuiunga mkono Taliban ndani ya Afghanistan na isiruhusu viongozi wa kundi hilo waitumie ardhi ya Pakistan kupanga mashambulio ndani ya Afghanistan.

Ameongeza kuwa Pakistan inapaswa itokemeze hifadhi na maficho ya kundi la Taliban ndani ya ardhi yake.

Mansour Ahmad Khan, balozi wa Pakistan nchini Afghanistan, ameliambia shirika la habari la Ufaransa kuwa, kuandaa makundi ya wanamgambo kwa ajili kukabiliana na Taliban kunaweza kuifanya hali ya Afghanistan iwe mbaya zaidi.

Kitambo nyuma, Pakistan iliahidi pia kwamba haitaruhusu ardhi yake itumike dhidi ya mtu yeyote.../ 

342/